Ujenzi wa Daraja la kisasa Wami lenye urefu wa mita 510 na upana wa mita 11.85 unaondelea wilayani Bagamoyo mkoani Pwani umefikia asilimia 56 ambapo unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2022.
Hayo yamesemwa na Mhandisi Mshauri wa Mradi huo Gabriel Sangusangu wakati akitoa maelezo kwa wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), waliotembelea kuona shughuli zinavyoendelea, na kusema kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutatatua changamoto za wananchi wa Bagamoyo.
Aidha ujenzi wa Daraja lenye njia mbili za magari, baiskeli na njia ya watembea miguu umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 67.7 ambazo ni fedha kutoka serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.
“Upana wa daraja hili umezingatia sehemu ya barabara, watembea kwa miguu pamoja na vizuizi kwa ajili ya usalama hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 56 matarajio yetu ni ifikapo Septemba, 2022 tutakuwa tumekamilisha,” Amesema.
Amesema ujenzi huo unajumuisha ujenzi wa barabara za maingilio ya daraja kwa pande zote mbili zenye jumla ya urefu wa kilomita 3.8 ambapo kilomita 2.1 kwa upande wa Kusini ya daraja na kilomita 1.7 kwa upande wa Kaskazini ili kuweza kuunganisha daraja jipya na barabara kuu ya Chalinze – Segera.
Hata hivyo Mkandarasi amekwishaleta asilimia 95 ya mitambo na vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya kazi ya ujenzi isipokuwa vile ambavyo kazi zake itafanyika baadae.