Kampuni ya DataVision International ambayo mwaka 2019 ilishinda tuzo ya ‘East Africa Brand Leadership 2019’ kama Kampuni bora zaidi katika utoaji wa huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), utafiti pamoja na utengenezaji wa mifumo ya malipo ya kielektroniki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, imesherehekea miaka 22 ya mafanikio, tangu kuanzishwa kwake.
Kila ifikapo Oktoba, Kampuni hiyo ya kizalendo yenye makazi yake Mikocheni jijini Dar es Salaam, husherehekea mwaka mmoja zaidi tangu ilipoasisiwa Oktoba, 1998.
Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Bw. Geofrey Mwaijonga amesema, “mafanikio na kuendelea kuwepo kwa DataVision International ni matokeo ya mchango wa akili na talanta za mamia katika kipindi chote cha mwaka,” amesema Mwaijonga.
“Tunafanya kazi bila kuchoka kuhakikisha kuwa kila mmoja wetu anatimiza jukumu lake katika kufanikisha malengo ya kampuni wakati wote. Kwa miaka mingi sasa, tumeweza kubadili muelekeo wa biashara yetu mara nyingi kutokana na utafiti wa kina uliofanywa kimkakati na washauri elekezi (consultants), tunaposherehekea miaka 22 ya mafanikio, ningependa kumshukuru kila mmoja kwa mchango wake katika kuhakikisha tunafika hapa, TUMEWEZA,” Mwaijonga ameongeza.
Kampuni hiyo imefanya kazi kwa mafanikio na taasisi za kitaifa, Serikali na taasisi za kimataifa, ikitoa ajira kwa maelfu ya watanzania na wageni.
Kati ya kazi ilizofanikisha mwaka huu ni pamoja na kuratibu Mfumo wa Kusimamia Sekta ya Ulinzi Binafsi (PSGP) na kubadili mfumo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzibar (ZHELB) kutumia mfumo na njia ya mtandao na kuachana na matumizi ya karatasi.