Kampuni ya DataVision International yenye makazi yake jijini Dar es Salaam, imeshinda tuzo ya ‘East Africa Brand Leadership 2019’ kama Kampuni Bora Zaidi katika utoaji wa huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), utafiti pamoja na utengenezaji wa mifumo ya malipo ya kielektroniki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Tuzo hizo zilitolewa Juni 19, 2019 jijini Dar es Salaam na Taasisi ya ‘World Marketing Progress’. Washindi walichaguliwa kati ya makampuni 100 yaliyokuwa yamependekezwa na watumiaji wa huduma husika kwenye vipengele mabalimbali kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
DataVision International ilitajwa kuwa mshindi katika kipengele cha Huduma za Ushauri wa Kitaalam (professional consulting services).
Kwa mujibu wa taasisi hiyo, utoaji wa tuzo hizo ulilenga katika kutambua makampuni, bidhaa, huduma au wafanyabiashara waliofanikiwa zaidi kwa uvumbuzi, ubunifu na ufanisi katika kulihudumia soko husika. Washindi walipatikana kupitia utafiti wa siri uliofanywa na taasisi hiyo uliowahusisha watu waliotumia bidhaa na huduma za makampuni husika katika nchi za Afrika Mashariki.
Afisa Mtendaji Mkuu wa DataVision International, Geofrey Mwaijonga alisema kuwa wameipokea tuzo hiyo kama heshima kwao na Taifa kwa ujumla, na kwamba tuzo hiyo ni kielelezo cha jinsi ambavyo kampuni hiyo imefanikiwa kutoa huduma bora zaidi kwa kila mdau wa huduma zake ndani na nje ya nchi.
“Tuzo hii ni kwa ajili ya wateja wetu ambao tunawathamini sana kwani wamekuwa wakituamini na kufanya nasi kazi tangu mwaka 1998, mwaka ambao DataVision International iliasisiwa. Pia, kwa upekee ulio sawa na huo, tunawashukuru wateja na washirika wetu duniani kote na tunapenda kuwaeleza kuwa tuzo hii ni kwa ajili yao pia,” alisema Mwaijonga.
“Pia, tunapenda kuwashukuru wafanyakazi wote wa Datavision International, waliopo na wale ambao waliwahi kufanya kazi nasi, tunawashukuru wote kwakuwa tuzo hii ni kielelezo halisi cha kazi yao nzuri waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya, kujituma, uadilifu na dhamira yao ya dhati katika kupata mafanikio,” Mtendaji Mkuu wa DataVision International aliongeza.
Hivi karibuni, DataVision International ilishiriki katika utoaji wa tuzo za kimataifa za ‘Global Learning X-Prize’ jijini Los Angeles nchini Marekani.
Kwa kipindi cha miaka 21 tangu kuanzishwa kwake, kampuni hiyo imekuwa ikitoa huduma kwa taasisi za kimataifa, taasisi za umma (Serikali) na taasisi binafsi.
Hivi sasa, kampuni hiyo kwa kushirikiana na vitengo mbalimbali vya Serikali inatengeneza mifumo ya Tehama kurasimisha sekta zisizo rasmi na kuongeza ufanisi. Kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, DataVision International wanafanya kazi ya kuwaorodhesha na kuwasajili wasanii kwenye mfumo maalum kupitia mradi wa Utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi unaofahamika kama TACIP.
Pia, DataVision International, kwa kupitia Jeshi la Polisi, inashirikiana na Chama Cha Sekta ya Ulinzi Binafsi Tanzania (TSIA) kuongeza ufanisi kisekta,wanaendesha mradi wa kusajili walinzi binafsi kwa njia ya kielektroniki kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Sekta ya Ulinzi Binafsi (PSGP).
Akifafanua kuhusu miradi ambayo DataVision Interantional inafanya kwa kushirikiana na vitengo mbalimbali vya Serikali, Mwaijonga amesema kuwa miradi wanayotekeleza imekuwa inalenga kutumia taaluma tulizonazo kuunga mkono kwa vitendo juhudi za kufikia malengo makuu ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo ni kuufikia uchumi wa kati kupitia kuongeza ufanisii katika utoaji wa huduma kwa kutumia TEHAMA na matokeo ya utafiti pamoja na kuongeza ajira ili kuboresha maisha ya kila Mtanzania.