Mlinda Lango David de Gea anaweza kustaafu soka ikiwa hatapokea ofa ifaayo ya kurejea kwenye mchezo, huku akisisitiza kutokuwa tayari kwenda Ligi ya Saudi Arabia.
Mhispania huyo bado hana klabu baada ya kuondoka Manchester United baadaya mkataba wake kufikia kikomo mwishoni mwa msimu uliopita mwezi Juni mwaka huu.
Alikuwa ameafikiana kuhusu mkataba mpya, lakini Mashetani Wekundu waliondoa ofa yao ya awali na kushindwa kukamilisha mpango wa kumsainisha mkataba mpya.
Taarifa zinaripoti kuwa, katika majira ya joto klabu za Bayern Munich na Real Madrid zilijadili uhamisho wa De Gea, ingawa hakuna hata mmoja aliyetuma ofa kwa kipa huyo.
Licha ya kuwaniwa na Klabu za Saudi Pro League na Qatari Stars League, imefahamika kuwa De Gea angependelea kusalia Ulaya na ameweka wazi hilo kwa washiriki wanaovutiwa kutoka Mashariki ya Kati.
Mchezaji mwenzake wa zamani wa Man Utd, Cristiano Ronaldo amekuwa akijaribu kumshawishi De Gea ajiunge naye Al Nassr, lakini kipa huyo habadiliki na msimamo wake wa sasa.
De Gea ana nia ya kucheza soka la Ligi ya Mabingwa Ulaya na yuko tayari kusubiri hadi dirisha la uhamisho la Januari litakapofunguliwa ili kuamua juu ya uhamisho wake mwingine.
Hata hivyo, ikiwa hatapokea ofa sahihi, vyanzo vimeeleza kuwa De Gea atafikiria kustaafu.
De Gea, ambaye anatimiza umri wa miaka 33 mwezi Novemba, ametumia maisha yake yote hadi kufikia hatua hii akiwa na klabu mbili pekee Atletico Madrid na kisha Man Utd.
Hajaichezea timu ya taifa ya Hispania tangu 2020 na aliachwa nje ya kikosi chao kwa Kombe la Dunia la FIFA la 2022.
Mrithi wake katika klabu ya Man Utd, Andre Onana, amekuwa na mwanzo mbaya wa maisha pale Old Traford, hivi majuzi zaidi akiruhusu bao wakati wa kichapo cha 4-3 kutoka kwa Bayern Munich kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano.