Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma Kanali, Simon Anange amesikitishwa na vitendo vya watoto kufanyiwa ukatili na ndugu na watu walioaminiwa kuwalea au kuwatunza iwe nje au majumbani kwao.
Ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya siku nne kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na Maafisa Ustawi wa Jamii kuhusu matumizi ya Kitini cha Malezi ya Mtoto na Familia yaliyotolewa na Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii, ambapo amesema kuwa asilimia 40 ya vitendo vya ukatili vinafanyika mashuleni ikiwemo utani wa kumdhalilisha mtu na kufanya watoto kuichukia shule.
Amesema kuwa ukatili wa kuwanyanyasa watoto haupaswi kufumbiwa macho, hivyo kila mmoja katika nafasi yake ahakikishe analinda haki na kujenga msingi bora wa mtoto ili kuweza kuondokana na tatizo hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Familia kutoka Wizara ya Afya, Idara Kuu Maendeleo ya Jamii, Grace Mwangwa amesema kuwa ili kuweza kuendeleza Jamii zetu Serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto imejipanga kutokomeza mila mbaya katika Jamii na kuenzi mila nzuri lakini pia kuitaka jamii kutambua kuwa kuna tofauti kati ya kutunza na kulea watoto.
Mafunzo hayo kuhusiana na malezi ya mtoto na familia yamefanyika kwa wataalamu wa maendeleo ya Jamii kutoka Mikoa ya Shinyanga, Kigoma na Katavi na mikoa hiyo kwa kiasi kikubwa ina changamoto ya uwepo wa mimba na ndoa za utotoni.