Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam, Saad Mtambule amewaongoza Wananchi wa Kata ya Kunduchi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali kufanya usafi maeneo ya fukwe ya Bahari ya Hindi.

Zoezi hilo, limefanyika pia kwenye magofu ya Kunduchi ikiwa ni sehemu ya ushiriki wa Maadhimisho ya siku ya usafi wa mazingira Duniani, huku akisema Serikali inatarajia kujenga dampo la kisasa eneo la  Mabwepande, ili kuimarisha masuala ya kimazingira, uzoaji wa taka na kuzichakata.

“Kupitia dampo hilo taka zinaenda kuwa mali kwa kuwa zinaenda kuzalisha ajira na inaweza kutengenezwa mbolea, gasi na bidhaa zingine mbalimbali, kwahiyo nitoe wito kwa wakazi wa Kinondoni kuhakikisha wanakuwa sehemu ya utunzaji mazingira ili yawe safi na salama muda wote.”

Kuhusu tahadhari ya kuwepo Mvua za El-nino, Mkuu huyo wa Wilaya amesema ni lazima kutunza mazingira kwa kuhakikisha yanakuwa safi na kuzibua mitaro ya maji machafu, ili mvua hizo zikija zisilete madhara.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Lions club, Happiness Nkya amesema taasisi hiyo imeungana na Dunia katika Maadhimisho hayo, ili kushiriki kufanya usafi wa mazingira.

Kwa upande wake Mwanzilishi wa Taasisi ya Mazingira Plus, Abdallah Mwikulu amesema wameitumia siku hiyo kutoa uelewa kwa jamii kuhusu mapambano ya kuondoa taka ngumu kwenye mazingira na kuongeza hamasa ya kufanya usafi hasa maeneo ya ufukwe.

Viongozi sikilizeni, tatueni kero za Wananchi - Rais Samia
Serikali yajipanga kupunguza uhaba wa Watumishi