Klabu ya West Ham United imeifungulia milango Klabu ya Arsenal ya kumsajili kiungo wao tegemezi Declan Rice huku ikitajwa kuwa ipo tayari kumuuza kwa timu yoyote itakayotoa dau lisilopungua Pauni 100 milioni katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Mkataba wa sasa baina ya timu hiyo na Rice umebakiza mwaka mmoja na miezi miwili na utafikia tamati mwishoni mwa msimu ujao ambapo nyota huyo wa England atakuwa huru kujiunga na timu nyingine.
Kutokana na hilo, West Ham United inaonekana haiko tayari kukosa fedha na mchezaji baada ya msimu ujao na hivyo inaripotiwa imeonyesha utayari wa kumruhusu Rice aondoke ili ipate fungu ambalo italitumia kuimarisha kikosi chake.
Ushawishi wa West Ham kwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 ili asaini mkataba mpya utakaomweka klabuni kwa muda mrefu unaonekana kugonga mwamba kutokana na Rice kuhitaji changamoto mpya katika timu kubwa zaidi na hivyo imelazimika kukubali kwa shingo upande kumtimizia ndoto yake.
Nyota huyo anaonekana kuhitaji kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini pia kushinda mataji jambo ambalo anaamini haliwezi kutimia akiwa na West Ham ambayo mashindano makubwa iliyowahi kushiriki ni yale ya Europa League.
Uamuzi wa kumuweka sokoni Rice hapana shaka utapokelewa vizuri na Arsenal ambayo imeonekana kuwa na hamu kubwa ya kumnasa mchezaji huyo wa zamani wa Chelsea ili kuimarisha zaidi safu yake ya kiungo.
Arsenal imekuwa ikimuwinda Rice tangu mwaka juzi baada ya kukoshwa na kiwango chake lakini ugumu ulikuwa ukiletwa na West Ham United ambayo ilionekana haiko tayari kumuachia nyota wake huyo anayemudu kucheza nafasi ya kiungo wa ulinzi na beki wa kati.
Mbali na Arsenal, timu nyingine ambazo zimekuwa zikimtolea udenda nyota huyo ni Manchester United, Liverpoll na Chelsea aliyowahi kuitumikia zamani.
Katika hatua hiyo ya nusu fainali, West itakutana na AZ Alkmaar ya Uholanzi na mshindi atakutana na timu itakayofuzu baina ya Fiorentina na FC Basel katika mchezo wa fainali utakaochezwa huko Prague, Jamhuri ya Czech, Juni 7.
Declan Rice amekuwa ni miongoni mwa nyota wa West Ham waliochangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya timu hiyo kwenye mashindano ya Europa Conference msimu huu ambapo ipo katika hatua ya Nusu Fainali, akicheza mechi nane na kupachika bao moja huku akipiga pasi moja ya mwisho..
Tangu alipoanza kukichezea kikosi cha wakubwa cha West Ham, msimu wa 2016/2017, Rice amecheza mechi 201, akipachika mabao tisa na kupiga pasi za mwisho 10, akionyeshwa kadi 26 za njano na hajawahi kupata kadi nyekundu.
Arsenal inataka kuimarisha safu yake ya kiungo na inamtaka Rice kama mbdala wa muda mrefu wa Granit Xhaka ambaye umri unaonekana kuanza kumtupa mkono na Thomas Partey ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.
Mchezaji mwingine ambaye Arsenal imekuwa ikimuwinda ni kiungo wa Brighton na timu ya taifa ya Ecuador, Moses Caiceido.