Uongozi wa klabu ya Manchester United umelalamikiwa kufanya maamuuza kwa haraka aliyekua mshambuliaji wao kutoka nchini Ubelgiji Romelu Menama Lukaku Bolingoli, kwenda Inter Milan kwa Pauni Milioni 74.
Lukaku aliondoka Manchester United majira ya kiangazi mwaka 2019, baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa misimu miwili, akitokea Everton.
Alipokua Manchester United alikabiliwa na changamoto ya kukosolewa kila kukicha, lakini bado alionyesha kiwango bora, huku akifunga mabao 42 katika michezo 96 aliyocheza.
Moja ya wadau wa soka duniani ambaye bado hajaelewa maamuzi ya uongozi wa klabu hiyo yenye mskani yake makuu Old Trafford United mpaka sasa, ni mshambuliaji wa Watford ya England Troy Deeney.
Mdau huyo amesema Manchester United walipaswa kusuburi kuhusu maamuzi ya kumuuza Lukaku, na anaamini kwa sasa wanajutia maamuzi waliyoyachukua, kutokana na mshambuliaji huyo kuonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kufumania nyavu za timu pinzani huko Italia.
Amesema kwa sasa Lukaku yupo vizuri, na hata waliokua wanamkosoa kila kukicha wameshindwa kuendelea na kejeli zao, hivyo anaamini kama angeendelea kubaki Old Trafford alikua na kila sababu ya kuonyesha makubwa zaidi.
“Yuko vizuri sana, na wakati wote niliona ulikuwa uamuzi mgeni sana United kuamua kuachana naye.”
“Tangia ameenda Italia unaweza kuona upande wa ufundi wake na upande wa kocha, amekuwa bora maradufu. Ana kitu cha kuthibitisha.”
Lukaku Inter
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, amekuwa na kiwango bora tangu alipoondoka Manchester United, ambapo kwa sasa ameshaifungia Inter Milan mabao 41 katika michezo 57 ya michuano yote aliyocheza. Miongoni mwa mabao aliofunga, 34 aliyapata msimu uliopita.
Kwa upande wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Lukaku ameendelea kuwa bora, kwani ameshapachika mabao 24 katika michezo 23, huku akitoa ushirikiano kwenye kikosi cha timu hiyo, wakati wa mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya England walioibuka na ushindi mabao mawili kwa sifuri.