Imebainika kuwa mlinda mlango Deogratius Munishi ‘Dida’, msimu ujao hatakuwa sehemu ya kikosi cha mabingwa wa kihistoria wa ligi kuu bara, Young Africans.
Hilo limebainishwa na kocha wa makipa wa klabu hiyo Juma Pondamali Mensah, wakati akifanya mahojiano na kipindi cha michezo cha Sports Leo kinachorushwa na kituo cha Radio One cha jijini Dar es Salaam.
Pondamali amesema wameamua kuachana na Dida baada ya kipa huyo wa zamani wa Simba SC na Azam FC kukataa kuongeza mkataba mpya akitaka asubiriwe mpaka hapo atakaporejea kutoka Afrika Kusini anakotarajia kwenda kwa ajili ya majaribio.
Pondamali amekwenda mbali zaidi, na kusema kuwa tayari Young Africans imeshaziba pengo la Dida kwa kumsajili kipa Mcameroon wa African Lyon, Youthe Rostand.
Kwa mujibu wa Pondamali ni kwamba msimu ujao Young Africans itakuwa na makipa watatu ambao ni Youthe Rostand, Beno Kakolanya pamoja na kipa mwingine mdogo ambaye hakutaka kumtaja jina.