Mchezaji wa Klabu ya Paris Saint-Germain, Angel Di Maria amemtupia lawama aliyekuwa Kocha wa Manchester United, Louis van Gaal kuwa alikuwa chanzo cha kuififisha nyota yake alipoichezea klabu hiyo mwaka 2014.
Di Maria alijiunga na wekundu hao wa Old Trafford mwaka 2014 akitokea Real Madrid kwa kitita cha £59.7, lakini aliichezea klabu hiyo kwa msimu mmoja tu akiambulia magoli manne pekee katika mechi 32 alizoshiriki.
‘Winga’ huyo aliyekimbilia PSG mwishoni mwa mwaka 2014, amedai kuwa kilichokuwa kinaendelea ndani ya klabu hiyo kuhusu kocha na wachezaji ndicho kilichomkwamisha kuonesha uwezo wake halisi.
-
Mnangagwa amuangukia Putin, ‘nisaidie kaka yangu’
-
Tyson Fury apewa nafasi ya kuzichapa na Anthony Joshua
“Nilikaa United kwa mwaka mmoja tu. Haukuwa muda mzuri kwenye maisha yangu ya soka, au tuseme sikuruhusiwa kutumia muda wangu bora zaidi kule,” Di Maria ameiambia France Bleu.
“Kulikuwa na matatizo na kocha aliyekuwepo (Van Gaal). Lakini namshukuru Mungu, niliweza kuondoka na kujiunga na PSG na kuonesha tena mimi ni nani,” aliongeza.
Di Maria akiwa na PSG wataikabili Manchester United inayong’ara sasa chini ya kocha wa muda Ole Gunnar Solskjær. Visiki hivyo vya soka vitakutana kwenye Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya hatua ya 16 bora.
Mchezaji huyo ameeleza kuwa anaelewa wanakutana na Manchester United iliyo na nguvu mpya na iliyojengwa upya, lakini watafanya jitihada za kujipatia ushindi katika mtanange huo.