Diamond Platinumz amemshauri Rayvanny ambaye ni msanii aliye chini ya lebo yake ya WCB na Harmonize ambaye alikuwa msanii wa kwanza kusainiwa na WCB na baadaye kutafuta njia yake, kufuatia mgogoro unaovuma kati yao.
Mkali huyo wa ‘Waah!’, amewataka wasanii hao ambao amewahi kuwalea, kujikita katika ushindani wa kimuziki na kuachana na ushindani wa maisha binafsi, kwani hakuwafunza hivyo.
Akizungumza na Wasafi TV hivi karibuni, Diamond amesema angependa kusikia wanashindana idadi ya wafuatiliaji wa kazi zao na ukubwa wa kazi zao, badala ya kupelekana polisi kwa masuala binafsi.
“Washindane katika ufanyaji wa kazi, washindane kwenye mambo mengine. Washindane kuona huyu ana views ngapi, huyu ana-subscribers wangapi… lakini sio mara tunasikia wanapelekana polisi. Sio kitu nilichowafunza,” Diamond ameiambia Wasafi TV.
Amewataka wasanii hao kuiga ushindani uliopo kati yake na Ali Kiba, ambao amesema umejikita katika kazi.
“Wakiangalia kama mfano kwetu sisi kaka zao, mimi na Ali Kiba, hawajawahi kusikia mara tumepelekana polisi. Tumekuwa tunashindana tu kwenye masuala ya kazi. Ndio kitu ambacho wananchi wanataka kusikia, tunataka maendeleo ya muziki,” amefunguka.
Diamond ambaye amesema anaenda nje ya nchi kwa ajili ya kukamilisha albam yake, amewatakia kila la heri Ray Vanny na Harmonize katika kazi zao za muziki.
Hivi karibuni kumekuwa na ‘vutankuvute’ kati ya Harmonize na Rayvanny, ambayo imehusisha tuhuma nzito za mapenzi. Wote walijikuta kwenye mtego wa tuhuma za kutaka au kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Paula ambaye ni mtoto wa Kajala na Paul Majani.
Harmonize ambaye alikuwa mpenzi wa Kajala, aliingia kwenye zengwe kuwa anataka ‘kula kuku na mayai yake’. Ikaelezwa kuwa anamtaka Paula huku akiwa na mama yake.
Awali, Ray Vanny alituhumiwa kujihusisha kimapenzi na Paula ambaye alirejewa kama ‘mtoto’, na kwamba anamrubuni.
Hata hivyo, bifu hilo limeingia pia kwenye reli ya muziki. Mengi yametokea baada ya Harmonize kuachia ‘Attitude’ akiwa na Awilo Longomba na H-Baba.
Endelea kutembelea Dar24 Media kuyapata mengi kwa undani.