Mlinda Lango chaguo la kwanza katika kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Diarra Djigui amewatuliza Mashabiki na Wanachama akiwaambia wasiwe na hofu.
Young Africans ilifungua pazia la Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2023/34 nchini Algeria, kwa kucheza dhidi ya CR Belouizdad iliyoshinda mabao 3-0, na mwishoni mwa juma hili itakuwa wenyeji wa Al Ahly iliyoanza kwa kishindo kwa kuifumua Medeama ya Ghana kwa mabao 3-0 jijini Cairo katika mechi nyingine ya Kundi B, huku Mlinda Lango Diarra aliyekosekana kwenye mchezo wa Algiers akisema kazi ndio imeanza na Mashabiki wa klabu hiyo hawapaswi kuwa na wasiwasi kutokana na matokeo ya ugenini.
Mlinda Lango huyo raia wa Mali alifunguka juu ya hali yake kwa kushindwa kudaka mechi hiyo ya kwanza, lakini akiwatoa hofu Mashabiki na Wanachama na kuwataka kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo ujao utakaopigwa Kwa Mkapa.
Diarra amesema anasumbuliwa na maumivu ya bega, licha ya kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Mali ambayo hata hivyo haikumtumia kwa vile ametakiwa kupata mapumziko zaidi ili kuwa kwenye hali nzuri ya kurudi uwanjani.
“Naendelea vizuri na ninafanya mazoezi na wenzangu, tatizo langu la bega halikuwa kubwa ila lilihitaji kupata mapumziko ya muda mrefu kiasi ili kujiweka hali nzuri ya ushindani nafikiri muda ukifika mtaniona uwanjani,”
“Siwezi kuweka wazi ni lini ila nipo kwenye hali nzuri mashabiki watarajie kuniona uwanjani muda wowote nafurahia upendo wao kwangu, nimepokea meseji nyingi ku ka kwa Wanayanga na ninawa-hakikishia hatutawaangusha.” Amesema Diarra
Kuhusu mechi iliyopita, Diarra amesema ulikuwa ni mzuri na wenye ushindani, lakini bahati haikuwa upande wao wamesahau matokeo hayo wanajipanga kwa mchezo muhimu zaidi wa Jumamosi (Desemba 02) dhidi ya Al Ahly.
“Tumepoteza, hii ni sehemu ya matokeo tumeumia, ila tunajipanga kwa mchezo mwingine ambao ni muhimu zaidi dhidi ya Al Ahly nyumbani hatuwezi kurudia makosa tunahitaji pointi zote tatu ili kurudi kwenye mstari na mashabiki wajiandae kupata ile burudani waliyoizoea,” amesema.
Diarra amesema wataingia kwenye mchezo huo kwa kuwaheshimu wapinzani wao hao, huku wakiwa na kumbukumbu ya maumivu ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa idadi kubwa ya mabao na kudai ndio soka lilivyo, hivyo mashabiki wasahau yaliyopita na kujitokeza kwa wingi.
“Tumepoteza, lakini sio mwisho wa michuano. Bado tuna nafasi ya kufanya vizuri nyumbani tumejifunza makosa hatuwezi kurudia, mashabiki wake kutupa nguvu,” amesema.