Beki wa Young Africans Dickson Job amekiri walifungwa bao kizembe dhidi ya AS Real Bamako, katika mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Young Africans ilicheza ugenini Bamako-Mali Jumapili (Februari 26), na kutangulia kupata bao la kuongoza kupitia kwa Mshambuliaji wao kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele, kabla ya wenyeji kusawazisha dakika za mwisho.
Job amesema bao walilofungwa ni sehemu ya makosa ambayo yanajirudia kwenye kikosi chao kinapokuwa katika mchezo wa mashindano, hivyo wanaendelea kuyafanyia kazi chini ya Kocha Nabi.
“Kweli tumeruhusu bao katika mchezo wetu dhidi ya AS Real Bamako kwa namna ile ile, kocha bado anaendelea kufanyia kazi kuhakikisha tatizo hili linakwisha kabisa.”
“Muda mwingine inatokea tu na mabadiliko yanayofanyika na mwili ukichangamka unajikuta umesahau kile ulichoelekezwa.” amesema Job
Young Africans ilirejea jijini Dar es salaam jana Jumanne (Februari 28), ikitokea Bamako-Mali ikipitia Adiss Ababa-Ethiopia.