Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Nasreddine Nabi amekanusha uvumi wa kuwa mbioni kuwa Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Nabi alikuwa akihusishwa kwenye mpango wa Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ ambalo lipo kwenye mchakato wa kumsaka Kocha Mkuuwa Taifa Stars.

Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema taarifa za kuhusishwa na Taifa Stars ameziona na kusikia katika Mitandao ya Kijamii, lakini ukweli ni kwamba hana mpango huo.

Amesema bado ataendelea kufanya kazi Young Africans kwa mujibu wa mkataba uliopo, na anaamini mikakati yake itatimia chini ya klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Nimeona hizo taarifa lakini hata familia yangu wameshtuka walipoona lakini niwashukuru wanaonifikiria kuhusu nafasi hiyo,”

“Naomba waambie mashabiki wa Young Africans kwamba Mimi kwa hapa Tanzania kwa sasa nitaifundisha timu yao pekee mpaka nitakapochukua uamuzi mwingine.”

“Sina maana kwamba kuifundisha Tanzania ni kazi mbaya kwangu hapana lakini huwa Nina utaratibu wa kumaliza jambo ambalo nimelianza,ningeweza kufikiria kitu kipya kama uongozi utaniambia ajira yangu hapa imefika mwisho.” amesema Nabi

Young Africans yahamia Chamazi
Dickson Job afunguka bao la Real Bamako