Rasmi mchezo wa 16 Bora Kombe la Shirikisho Tanzania Barani ‘ASFC’ kati ya Mabingwa watetezi Young Africans dhidi ya Maafande wa Jeshi la Magereza Tanzania Prisons utachezwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Young Africans ambao watakuwa wenyeji wa mchezo huo utakaoanza saa moja usiku, wamethibitisha kupitia mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika leo Jumatano (Machi Mosi), Makao Makuu ya Klabu hiyo jijini Dar es salaam.

Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe amesema mchezo huo umelazimika kupelekwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi, kufuatia Uwanja wa Benjamin Mkapa kufungwa kwa muda, kupisha maboresho ya sehemu ya kuchezea ‘Pitch’.

“Mchezo wetu dhidi ya Tanzania Prisons wa Kombe la TFF utachezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex pale Chamanzi, hii imekuja baada ya Uwanja wetu wa nyumbani Benjamin Mkapa kuwa katika Ukarabati”

“Kwa hiyo sisi tumeuchagua Uwanja wa Azam Complex kwaajili ya mechi yetu ijayo dhidi ya Tz Prisons na mechi nyingine za Ligi Kuu, na mechi za Kimataifa zitachezwa Benjamini Mkapa” amesema Ally Kamwe

Tayari Simba SC imeshathibitisha mchezo wake wa 16 Bora Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Africans Sports, utachezwa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, kesho Alhamis (Machi 02).

Chalamila: Viwanja visivyoendelezwa vifutwe
Kocha Nabi aikana TFF, Taifa Stars