Gwiji wa soka duniani, Diego Armando Maradona ametangazwa kuwa kocha wa klabu ya Dorados inayoshiriki ligi daraja la pili nchini Mexico.
Uongozi wa klabu ya Dorados umethibitisha kumtangaza Maradona kupitia picha ya video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, iliyonakshiwa ujumbe usemao ‘Karibu Diego’, ‘Na uifanye kuwa namba 10’, wakimaanisha aibebe klabu hiyo kama alivyoitendea haki jezi namba 10 alipokua akicheza soka.
Mbali na kusambaa kwa video hivyo katika mitandao ya kijamii, pia baadhi ya vyombo vya habari nchini Mexico vimeeleza kuwa uongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake makuu mjini Sinaloa, umemtangaza Maradona baada ya kumtimua aliyekua kocha klabuni hapo Francisco Gamez.
Klabu ya Dorados ilimtimua Gamez mapema jana Alhamisi, baada ya kuwa na mwanzo mbaya katika ligi daraja la pili nchini Mexico, ambapo mpaka mwishoni mwa juma lililopita alikua amefanikisha upatikanaji wa alama 3 katika michezo 5 waliyocheza.
Klabu hiyo inakamata nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi daraja la pili nchini Mexico, yenye timu 15.
Maradona mwenye umri wa miaka 57, anakumbukwa kwa mazuri aliyoyafanya akiwa mchezaji na nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya Argentina kilichofanikiwa kutwaa ubingwa wa dunia mwaka 1986, baada ya kuifunga Ujerumani.
Amewahi kuzinoa baadhi ya klabu nchini kwao Argentina na Umoja wa Nchi za falme za kiarabu (UAE), lakini jambo kubwa katika tasnia ya ukufunzi ni kuingoza timu ya taifa lake kama kocha wakati wa fainali za kombe la dunia mwaka 2010.