Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameagiza Tume ya Mipango nchini kuweka uratibu wa ushiriki wa makundi mbalimbali ya wananchi na Wadau wengine katika kutoa maoni kwenye mchakato unaoendelea wa uandaaji Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050.
Biteko ameyasema hayo wakati akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la kwanza la Wanamipango 2023 iliyofanyika tarehe 27 Novemba 2023 jijini Arusha.
Amesema, “Tume ya Mipango hakikisheni Wananchi wote wanashiriki kikamilifu kutoa maoni yao kuhusu Tanzania wanayoitaka katika miaka 25 ijayo, maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 yameanza na kutokana na umuhimu wa Dira kwa Taifa letu, wanamipango na wadau wote ni muhimu kila mmoja kwa nafasi yake ashiriki kikamilifu katika hatua zote za maandalizi kama atakavyohitajika.”
Biteko ameongeza kuwa, Maafisa Mipango pia wanatakiwa kubadilika na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya Miradi na Programu zote zinazotekelezwa katika maeneo yao ikiwemo zinazofadhiliwa na Wadau wa Maendeleo badala ya ile inayogharamiwa na Serikali Kuu au Halmashauri pekeehuku akielekeza Wakurugenzi wa Mipango kuzingatia utamaduni wa kuwa na mawazo ya pamoja katika kupanga mipango ya Serikali na nchi kwa ujumla ili kuleta mipango imara itakayosaidia Taifa kufikia uchumi wa juu.
“Wanamipango waliopewa jukumu la kusimamia miradi pamoja na ufuatiliaji na tathmini kuzingatia utaratibu wa kutoa taarifa za utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo inayotekelezwa. Shughuli za tathmini na ufuatiliaji ni muhimu nchini hivyo zinapaswa kupewa kipaumbele cha kutengewa rasilimali za kutosha,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, amewataka Maafisa Mipango kuona thamani ya kada yao na wahakikishe kuwa wanakuwa wafuatiliaji wakubwa katika upangaji wa mipango kutoka ngazi ya chini hadi Taifa, kwa ajili ya manufaa ya nchi ambapo pia amewaagiza Wakurugenzi wa Sera na Mipango kuhakikisha kuwa wanaweka mipango inayotekelezeka kwa manufaaa ya nchi kiuchumi.
Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela.