Dirisha la rufaa kwa wanafunzi ambao hawajaridhika na viwango vya mikopo walivyopangiwa, limefunguliwa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), ili kutoa nafasi ya kuwasilisha taarifa za uthibitisho na kuongezewa viwango vya mikopo kulingana na uhitaji wao kwa watakaokidhi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru iliyotolewa hii leo Novemba 13, 2022 imesema dirisha hilo la rufaa litakuwa wazi kwa siku saba kuanzia leo hadi Jumapili ijayo na kwamba tayari wanafunzi 68,422 wa mwaka wa kwanza wamepangiwa mikopo.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru.

Amesema, “Hadi leo Novemba 13, 2022, tumeshawapangia mikopo wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 68,422 na tunafahamu kuwa kuna wanafunzi ambao kwa sababu mbalimbali, hawakukamilisha nyaraka muhimu kuthibitisha uhitaji wao, dirisha la rufaa ni fursa kwao.”

Aidha Badru ameongeza kuwa, lengo la HESLB ni kutoa mikopo kwa wanafunzi wapya 71,000 katika mwaka wa masomo 2022/2023 na kuwasihi wanafunzi wanaowasilisha rufaa kusoma na kuzingatia maelekezo yaliyopo kwenye mfumo wa kuwasilisha rufaa huku akiwataka wanafunzi waliopangiwa mikopo kufika kwa maofisa mikopo wa vyuo vyao ili kukamilisha taratibu.

DC amuomba Rais Samia Gari la Zimamoto
Mitihani Kidato cha nne: Watahiniwa 566,840 kujiuliza kesho