Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mwakilishi wa wananchi katika Baraza/Mkutano la Kaunti (MCA) ya Homa Bay nchini Kenya, Godfrey Anyango amevuliwa nguo kwenye mkutano wa baraza baada ya kutokea ‘vutanikuvute’.
Kwa Kenya, Members of The County Assembly (MCA) ni mwakilishi wa Kaunti, kama ilivyo kwa madiwani ambao ni wawakilishi wa Kata nchini Tanzania.
Citizen wameripoti kuwa tukio hilo lilitokea jana, Agosti 18, 2020 mchana, baada ya kutokea vurugu kati ya wajumbe. Imeeripotiwa kuwa wajumbe wengi walikuwa wanapinga hoja ya kutaka kumuondoa Katibu wa Kaunti hiyo, Daniel Kaudo anayekabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma.
Wajumbe hao walipinga hoja hiyo wakidai kuwa utaratibu haukufuatwa na wakataka iondolewe mbele ya baraza.
Onyango alisimama akauliza inakuwaje mtu ambaye sio mjumbe wa Bodi ya Baraza hilo aongoze hoja ya kumuondoa Katibu. Alidai kuwa hoja hiyo ilipaswa kuwasilishwa na mjumbe ambaye ana sifa za kukaa kwenye Bodi ya Baraza la Kaunti.
Wajumbe wengine (MCAs) na kaunti zao kwenye mabado, Evance Marieba (Gwassi North), Walter Muok (Kanyadoto) na Paul Adika (Lambwe) walisimama wakimuunga mkono Anyango, wakihoji kwanini Spika Elizabeth Ayoo hataki kuruhusu wajumbe wenye maoni tofauti kutoa maoni yao.
Citizen imeripoti kuwa wakati mvutano huo wa hoja ukiendelea, kundi la wajumbe wanne walienda moja kwa moja kwa Anyango na kumshambulia.
“Walimshabulia kwa kumpiga ngumi, mateke na baadaye kumvua nguo,” citizen imeripoti.
Kwa dakika kadhaa, mkutano uligeuka kuwa ukumbi wa ndondi zisizo na maelekezo, wajumbe wakishambuliana kwa ngumi na mateke huku wajumbe wanawake wakijificha.