Mlinda Lango chaguo la Kwanza Young Africans Djigui Diarra, ameahidi kuendelea kufanya vizuri katika michuano ya ndani nan je ya Tanzania msimu ujao 2023/24.
Diarra raia wa Mali ametoa kauli hiyo, baada ya kukabidhiwa dola za Marekani 4200 (zaidi ya sh. milioni 10) na msanii wa bongo fleva, Nassibu Abdul ‘Diamond Platnumz, alizomuahidi kutokana na kiwango bora alichokionyesha katika mchezo wa pili wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger.
Katika mchezo huo uliochezwa mwishoni mwa wiki, Yanga ilishinda bao 1-0 katika Uwanja wa 5 Julai 1962 nchini Algeria huku Diarra akionyesha kiwango kikubwa kwa kuokoa mashambulizi ya hatari ikiwemo mkwaju wa Penati.
Wakati mchezo huo ukiendelea, Diamond aliahidi kuwa atampa zawadi kipa huyo bila ya kujali matokeo ya mwisho ya mechi, ambapo jana alitimiza ahadi yake.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fedha hizo, Diarra alimshukuru Diamond na kuahidi ataendelea kufanya vizuri zaidi katika timu hiyo.
Alikiri motisha ambayo wanaendelea kupata imekuwa chachu ya kufanya vyema katika mashindano mbalimbali.
“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mchango mkubwa ambao ametupatia wachezaji hadi kufikia hapa. Namshukuru Diamond kwa sapoti aliyoonyesha,” alisema.
Mlinda Lango huyo huyo ameahidi kikosi chao kitapambana kuhakikisha kinashibda mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Azam FC.