Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amefichua kuwa, kufanya vizuri kwa Young Africans katika michuano ya kimataifa, kumepelekea aongeze umakini mkubwa katika machaguo ya wachezaji anaowahitaji kwenye kikosi chake kwa lengo la kufanya makubwa katika Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu ujao 2023/24.

Robertinho ametoa kauli hiyo, huku ikiwa tayari Simba SC imetangaza kuachana na kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ghana, Agustine Okrah kutokana na kushindwa kufikia malengo ya timu hiyo msimu huu 2022/23.

Akizungumza jijini Dar es salaam Robertinho amesema, malengo yake yapo katika kuhakikisha Simba SC inafanya usajili wa maana kuelekea msimu ujao ili waweze kufikia malengo makubwa kama ilivyokuwa kwa wapinzani wao Young Africans.

“Tunamalizia Ligi Kuu msimu huu, kisha tutaanza msimu ujao kwa kufanya usajili halafu maandalizi yatafuata, kwa sababu malengo yetu bado ni makubwa baada ya kushindwa kuyafikia msimu huu, maana ukiangalia hakuna kombe lolote ambalo tumelipata.

“Nadhani kuna haja ya kuwa makini katika usajili kwa kuhakikisha napata kile ambacho ninakiomba kutokana na mahitaji ya timu kuelekea msimu mpya kuanzia ligi ya ndani na michuano ya kimataifa, kwa sababu kila mmoja ameona namna wapinzani wetu (Young Africans) walivyofaidika kutokana na kuwa na kikosi kizuri,” amesema Robertinho.

Ikumbukwe kuwa, msimu huu, Young Africans imeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo mwaka 2004, ambapo ilipoteza mbele ya USM Alger ya Algeria Jumamosi (Juni 03) kwa kanuni ya bao la ugenini.

Wabunge watakaopinga harakati za rais kukiona
Djigui Diarra: 2023/24 tutakiwasha zaidi