Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amefanya ziara ya kikazi katika Kisiwa cha Songosongo mkoani Lindi kwa lengo la kukagua maendeleo ya kazi za uzalishaji na uchakataji wa Gesi Asilia ambayo husafirishwa na kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo uzalishaji umeme.
Ziara hiyo imefanyika hii leo Novemba 13, 2023 ambapo pamoja na kukagua visima vya gesi vilivyopo baharini na nchi kavu, pia alizungumza na Wafanyakazi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kampuni yake tanzu ya GASCO na Wananchi katika Kata na Kijiji cha Songosongo.
Baada ya kukagua na kuona hali halisi ya visima vya Gesi Asilia na mitambo ya kuchakata gesi hiyo, Dkt. Biteko amewataka watendaji wa TPDC kusimamia kikamilifu kampuni zinazozalisha Gesi Asilia ili muda wote nchi iwe na gesi ya kutosha.
Aidha, amewapongeza Wafanyakazi wa kampuni ya TPDC na GASCO, kwa kazi nzuri wanayofanya ambayo imepelekea asilimia 65 ya umeme unaozalishwa nchini utokane na gesi hiyo na amewataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii.
Awali, Wananchi katika Kata ya Songosongo walimweleza Naibu Waziri Mkuu changamoto mbalimbali walizonazo ikiwemo ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kwani kwa sasa wanapata umeme kutoka kampuni ya Songas yenye visima vya gesi katika kata hiyo, hata hivyo umeme huo haujasambaa kwa wananchi wote takriban 5000 na hautoshelezi mahitaji.
Kutokana na hilo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ameuagiza Wakala wa Nishati Vijijini ( REA) wiki ijayo kufika kisiwani hapo ili kufanya tathmini ya upelekaji umeme katika Kisiwa hicho ili wananchi hao wasambaziwe umeme.
Katika hatua nyingine, wananchi hao walimweleza Dkt. Biteko kuwa, kwa sasa wanapata maji safi kiasi cha lita 100,000 kwa siku kutoka TPDC na Songas lakin bado kuna changamoto ya kupata maji ya kutosha suala ambalo Dkt. Biteko aliwaagiza TPDC kushughulikia suala hilo ikiwa ni sehemu ya utoaji huduma kwa wananchi wanaozunguka mradi.
Katika ziara hiyo, Dkt.Biteko aliambatana na viongozi mbalimbali akiwemo, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Michael Mjinja, na Mkurugenzi wa TPDC, Mussa Makame.