Nimepokea kwa mshituko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Bernard Kamillius Membe. Nimemfahamu miaka mingi, tumetoka nae mbali na tumesaidiana kwa mengi. Familia zetu, na mapito ya maisha yetu yamehusiana sana.
Bemard Kamillius Membe alikuwa ni mtu wa msaada mkubwa kwangu katika maisha yangu ya kikazi na kisiasa.
Nilimuamini na kumtumainia katika nafasi zote alizohudumu kwenye Baraza langu la Mawaziri. Aliwahi kuwa Naibu Waziri katika Wizara
ya Mambo ya Ndani, na Wizara ya Nishati na Madini. Halikadhalika, aliwahi kuwa Waziri wangu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka 9 ambapo alifanya kazi kubwa na nzuri ya kuendeleza maslahi ya Tanzania katika medani za Kimataifa.
Nautambua mchango wake mkubwa alioutoa kwenye Chama Cha Mapinduzi alipokuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Mjumbe wa Kamati Kuu na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa katika Sekretariati ya Halmashauri Kuu ya Taifa.
Katika nafasi zote hizo, alijitoa kwa moyo wake wote na kuacha alama za kudumu.
Nilimfahamu Mheshimiwa Membe kama Mwanadiplomasia Mbobezi, Mwanamikakati makini, Msomi mzuri, Mcha Mungu, Mzalendo, Mchapakazi Hodari na mtu jasiri ambaye hakuogopa kusema na kulisimamia analoliamini. Hakika Taifa limepoteza mmoja wa watu wake muhimu.
Natoa salaam za rambirambi na mkono wa pole kwako Shemeji yangu Dorcas Membe na watoto wenu Cecilia, Richard na Dennis, pamoja na wajukuu, ndugu na jamaa wa Marehemu Bernard Kamillius Membe. Nawapeni pole kwa msiba mkubwa uliowakuta, lakini napenda kuwahakikishia kuwa hamko wapweke.
Mimi pamoja na Mke wangu Salma na wana familia wetu wote, tuko pamoja nanyi katika majonzi na kuomboleza. Tunawaombea kwa Mola awajalie moyo wa subira na ustahamilivu katika kipindi hiki kigumu mnachopitia.
Tukumbuke daima, “Sisi sote ni waja wake, na kwake tutarejea”. Bwana ametoa, Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.
Tumuombee kwa mola marehemu mpendwa wetu, apumzike kwa amani na Roho yake aiweke Mahala Pema Peponi.
Amina.