Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), leo imemkabidhi Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Ripoti ya Tathmini ya Utendaji Kazi ya Mwaka wa Fedha 2017/18, ambayo ndani yake ina taarifa ya Ukaguzi wa ununuzi wa Umma kwa Mwaka wa Fedha husika.
Ripoti hiyo imekabidhiwa jijini Dodoma kwa Waziri Dkt. Mpango na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA Balozi Dkt. Matern Lumbanga aliyekuwa ameambatana na wajumbe wa Bodi na Menejimenti.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Ripoti hiyo, Waziri Dkt. Mpango ameipongeza PPRA kwa kazi iliyoifanya akieleza kuwa ni kazi muhimu kwa taifa.
“Nikupongeze sana [Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA] na timu yako, kwa kazi hii muhimu sana katika usimamizi wa ununuzi wa umma katika taifa letu. Hii ni kazi muhimu sana. Mmefanya kazi nzuri na ninawapongeza kwa dhati kabisa,” alisema Dkt. Mpango.
Aidha, Dkt. Mpango aliiahidi Bodi ya PPRA kuwa ripoti hiyo itafanyiwa kazi na kwamba wote waliobainika kutofuata taratibu za ununuzi watachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Mimi nilijifunza kwamba kama mtu anafanya kosa halafu hakuna kinachotokea, hatutapata tiba. Kwa hiyo ningependa kuona hatua za kinidhamu kwa wahusika zinachukuliwa. Wakuu wa taasisi wachukue hatua za kinidhamu; na hata wale ambao inabidi wapelekwe kwenye vyombo vya sheria, ifanyike hivyo,” alisema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango pia alielekeza PPRA kuendelea kutoa mafunzo ya kujenga uwezo kwa Taasisi za Umma pamoja na kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.
Akizungumza kabla ya kukabidhi ripoti hiyo, Mwenyekiti wa PPRA, Dkt. Matern Lumbanga alisema kuwa Mamlaka hiyo ilifanya ukaguzi wa mikataba 3,763 yenye thamani ya shilingi bilioni 805.68 na kwamba kiwango cha wastani wa uzingatiaji wa sheria kilikuwa asilimia 74.
“Kati ya taasisi 60 zilizokaguliwa, 11 ni taasisi zenye ununuzi mkubwa zaidi ambazo jumla ya ununuzi wake ni shilingi bilioni 403.72. Taasisi hizo zilipata wastani wa jumla wa asilimia 72,” alisema Dkt. Lumbanga.
Katika hatua nyingine, Dkt. Lumbanga alisema kuwa katika kuboresha mfumo wa usimamizi wa ununuzi wa umma, Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Umma inafanya majaribio ya Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Mtandao (TANePS), uliozinduliwa rasmi mwezi Juni, 2018 na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa.
Alisema kwa sasa mfumo huo unafanyiwa majaribio kwenye taasisi 100 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba pamoja na huduma mtambuka, ambapo jumla ya wazabuni 730 walisajiliwa kwenye mfumo huo katika mwaka huo wa fedha, lengo likiwa ni kuhakikisha manunuzi yote yanafanywa kwa njia ya mtandao.
Waziri Dkt. Mpango ameahidi kuwasilisha ripoti hiyo katika kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria.