Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Burundi kuwekeza Tanzania kutokana na mazingira bora ya biashara yaliopo na kwamba Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza mitaji yao.
Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati akifanya mazungumzo na Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka nchini Burundi wenye lengo la kuwekeza nchini Tanzania wakati alipowasili katika mji wa Bujumbura nchini Burundi kuhudhuria Mkutano wa Dharura wa 21 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki – EAC.
Amesema, tangu kuingia madarakani Serikali imeweka mkazo katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwemo kuhakikisha inatatua changamoto za wafanyabishara kwa lengo la kukuza na kuimarisha biashara na uwekezaji.
Ameongeza kuwamba hali ya uchumi nchini Tanzania inaendelea vizuri ikihusisha kufanya jitihada kubwa kusimamia sera za fedha na sera za kibajeti na kuhakikisha usalama wa chakula unakuwepo na kutaja hatua zingine kuwa ni kudhibiti mfumuko wa bei ambapo mpaka sasa nchini Tanzania mfumuko huo upo chini ya asilimia 5, kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni pamoja na kufanya vikao vya pamoja vya Rais na wafanyabiashara ili kutatua changamoto zao.
Aidha, Makamu wa Rais amesema ipo fursa nzuri zaidi ya kufanya biashara baina ya nchi majirani na za kikanda kwa kutumia ukanda huru wa biashara barani Afrika (AfCFTA), na kuwaelekeza wawekezaji hao jitihada zinazofanywa na Tanzania katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo Reli, Barabara na Viwanja vya Ndege ambayo itarahisisha biashara kwa wawekezaji wa mataifa hayo mawili.
Makamu wa Rais ameipongeza benki ya CRDB kwa utoaji wa huduma za kifedha nchini Burundi na kuzitaka taasisi za serikali ikiwemo bandari kuhakikisha zinawahudumia vema wawekezaji. Aidha amewasihi wawekezaji hao kutumia ubalozi wa Tanzania nchini Burundi wakati wanapopata changamoto ili ziweze kuwasilishwa kwa taasisi husika na kushughulikiwa kwa haraka.