Katika kuhakikisha kuwa Serikali inawajali wafanyabiashara ndogo ndogo, maarufu kwa jina la (Machinga) Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amewahakikishia wafanyabiashara wadogo kuwa Serikali itaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Ameyasema hayo mara baada ya kukagua zoezi la usajili wa wafanyabiashara hao linaloendelea katika Ofisi za TRA Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam ambapo ameshuhudia idadi kubwa ya wafanyabiashara hao wakiwemo waendesha bodaboda, mamalishe na wauza bidhaa mbalimbali wakiendelea kujisajili ili wapate vitambulisho.

Amesema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuwawekea wafanyabiashara hao wadogo wadogo utaratibu mzuri ili waendelee kufanya kazi zao za kujenga familia na Taifa kwa ujumla bila bughudha kwa kuwa Serikali inathamini mchango wao katika uchumi na maendeleo ya nchi.

“Nawasihi mkawaeleze Watanzania wengine na wafanyabiashara ndogo ndogo wenzenu wajitokeze kwa wingi kujiandikisha ili wasajiliwe na kupewa vitambulisho vitakavyowasaidia kujulikana”alisisitiza Dkt. Mpango

Aidha, Dkt. Mpango ameitolea mfano nchi ya Sweden kwamba imeweka utaratibu mzuri wa masoko maalumu kwa ajili ya wamachinga wao kila siku za Jumamosi na Jumapili ambapo watu wengi hufika maeneo hayo kununua bidhaa hali inayoashiria kuwa suala la uwepo wa wafanyabiashara wadogo wadogo ni la nchi nyingi duniani.

Hata hivyo, amewapongeza Watanzania wote kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kujitokeza kwa wingi kulipa kodi mbalimbali ikiwemo kodi ya majengo kwa kuwa kodi hizo zinaipa Serikali nguvu na uwezo wa kuwahudumia ipasavyo.

 

TFF Yaanika Mambo Hadharani
Florentino Perez aweka wazi anavyomhusudu Eden Hazard