Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema kukamilika kwa ujenzi barabara ya Kabingo- Kasulu- Manyovu kutafungua mkoa wa Kigoma kiuchumi na biashara baina ya mkoa huo na mikoa mingine pamoja na nchi jirani.
Makamu wa Rais amesema hayo akiwa eneo la Busunzu wilayani Kibondo mkoani Kigoma leo tarehe 22 Machi 2023 wakati akizungumza na kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma inayokagua maendeleo ya ujenzi wa miradi mbalimbali mkoani humo.
Makamu wa Rais pia ameuagiza Wakala wa Barabara Nchini – TANROAD, kumsimamia mkandarasi kikamilifu ili kuhakikisha barabara hiyo ya kilometa 260.6 inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili. Aidha ametoa rai kwa serikali ya mkoa wa Kigoma kusimamia vema miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.
Awali, Mwenyekiti kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, Jerry Silaa aliipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa na wenye tija katika mkoa huo ambao utaleta manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi. Amesema kwa sasa wameshuhudia mkoa huo ukipiga hatua za maendeleo katika sekta za nishati na miundombinu kama reli na barabara.