Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekutana na Makamu wa Rais wa Uganda, Jessica Alupo pamoja na ujumbe wa Wizara ya Kilimo ya Cuba ukiongozwa na Naibu wa Wizara hiyo, Bernado.
Rais Dk Mwinyi katika mazungumzo hayo alimshawishi Makamu huyo wa Rais wa Uganda nchi yake ianze kutumia viuadudu, dawa inayotengenezwa Kibaha, Mkoa wa Pwani na kiwanda kinachotumia teknolojia kutoka kwa wataalamu wa Cuba, kwa ajili ya kuangamiza vimelea vya mbu ili kuangamiza Malaria.
Rais Dkt. Mwinyi alimueleza Makamu huyo wa Rais wa Uganda kwamba kiwanda hicho kilianza uzalishaji wa viuadudu tangu mwaka 2017 na kwambaNchi kadha za Afrika zimenufaika na dawa hiyo ya viuadudu kutoka Kibaha ikiwemo Niger, Angola, Msumbiji na Eswatini.
Aidha, Dkt. Mwinyi pia alimueleza Makamu Jessica Alupo kwamba mbali ya kutengeneza viuadudu kiwanda hicho teknolojia yake kinaweza kutengeneza pia mbolea.
Baada ya Maelezo hayo Makamu wa Rais wa Uganda alionesha kuvutiwa na bidhaa hiyo na kueleza kwa vile nchi yake inasumbuliwa na Malaria wapo tayari kutumia bidhaa hiyo itakayosaidia kuondokana na vifo vya watoto na kina mama vinavyotokana na Malaria.
Kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Rais Dk. Mwinyi aliahidi kuigawia bure Uganda lita elfu moja za dawa hiyo ili waijaribu na baadae wapeleke wataalam wao wa Afya kuangalia teknolojia ya kuzalisha dawa hiyo ombi lililokubaliwa na Makamu wa Rais wa Uganda Jessica Alupo.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba, Bernado alieleza wamesaidia kuingiza teknolojia ya dawa ya viuadudu ili kusaidia mapambano dhidi ya Malaria Afrika.
Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Steve Byabato na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole.