Dkt. Hussein Mwinyi aliyepitishwa kugombea urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), leo asubuhi anatarajia kuchukua fomu ya kugombea urais katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM (Zanzibar), Catherine Peter Nao amewaambia waandishi wa habari visiwani humo kuwa baada ya kuchukua fomu hizo katika ofisi ya ZEC, Dkt. Mwinyi ataungana na wanachama wa chama hicho katika Ofisi za Kisiwandui.
“Tunawakaribisha wanachama na wasio wanachama wa CCM kuungana na Rais wao ajaye kwa ajili ya siku hii kubwa,” Nao anakaririwa.
Akizungumzia hali ya uchaguzi wa mwaka huu, amewataka wanasiasa wote kuhakikisha wanafanya siasa za kistaarabu zinazozingatia hali ya usalama wa nchi.
“Tuna ilani nzuri ya uchaguzi ambayo tunaamini kabisa itavuta mioyo ya Watanzania,” amesema.
Kiongozi huyo wa CCM alisisitiza kuwa wana mgombea ambaye anakubalika kwa wananchi na anauzika kirahisi. Hivyo, wanaamini eneo hilo la Kisiwandui lenye uwezo wa kuchukua watu 50,000 litajaa leo.
Ameongeza kuwa wanatarajia kushinda uchauguzi mkuu kwa asilimia 85 visiwani Zanzibar na asilimia 95 katika Tanzania Bara.