Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameibeba kwa dhati ajenda ya matumizi ya Nishati mbadala, kutokana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Kapinga amesema hayo wakati wa Baraza Maalum la Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi – UVCCM, Mkoa wa Ruvuma, sanjari na ugawaji wa majiko/mitungi ya gesi yaliyotolewa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga.

Amesema, “nyote mnafahamu ajenda ya Rais kuhusiana na umuhimu wa nishati mbadala, tunafahamu changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na changamoto za mazingira kwa ujumla, tunaanza mchakato wa kuelimisha Watanzania ili kuondokana na nishati ambazo sio rafiki kwa mazingira, na kutumia zilizo rafiki kwa mazingira.”

Aidha, Naibu Waziri Kapinga ambaye pia ni Mbunge wa Vijana Mkoa wa Ruvuma amewataka Vijana kushirikiana na Wanawake, Wazee na makundi mengine kuhakikisha wanapunguza changamoto za kimazingira kwa matumizi ya Nishati mbadala.

Awali, akiwasilisha Mada kuhusu nishati safi ya kupikia, Mhandisi Kelvin Tarimo kutoka REA amesema wanaendeshwa kwa mipango ya Sera ya Taifa wa Upelekaji Nishati Vijijini, Mpango wa usambazaji wa huduma ya umeme vijijini na Mpango wa Nishati safi za kupikia.

Sir Jim Ratcliffe aitikisa kivingine Man Utd
Neema yabisha hodi kwa Mabaharia wa Tanzania Kimataifa