Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameondoa zuio la kufanya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa kwa madai kuwa ni haki yao kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.
Ameyasema hayo leo leo Januari 3, 2023 Ikulu Jijini Dar Es Salaam wakati akizungumza na viongozi wa kitaifa wa vyama mbalimbali vya siasa.
“Wajibu wenu ni kufuata sheria zinavyosema ni kufuata kanuni zinavyosema, lakini kama waungwana kama wastaarabu Watanzania wenye sifa ndani ya dunia hii niwaombe sana, tunatoa ruhusa twendeni tukafanye siasa za kistaarabu, siasa za kupevuka, tukafanye siasa za kujenga sio kubomoa,” amesema Dk Samia.
Rais Samia amesema mikutano hiyo kisheria, ni haki haki kwa vyama vya siasa kuiendesha huku akisema kwa upande wa Serikali wamejipanga kutekeleza wajibu wao wa kulinda mikutano hiyo.
Aidha amesema kuwa jukumu sasa linabaki kwa vyama vya siasa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola kama sheria na kanuni zinavyoelekeza ili vipatiwe ulinzi.
“Ruhusa ya mikutano ya kisiasa itatolewa, wajibu wetu sisi Serikali ni kuwalinda mfanye mikutano yenu salama mmalize vizuri, kufuata kanuni ndio wajibu wenu vyama vya siasa,” amesema.
“Ni haki kwa vyama vya siasa kuendesha mikutano ya hadhara, kwa upande wa serikali tumeshajipanga, wajibu wetu ni kulinda mikutano ya vyama vya siasa, wajibu wenu vyama vya siasa ni kutupa taarifa kama sheria na kanuni zinavyosema kisha vyombo vinatoa ruhusa,” amesema.
Rais amesema hatua waliyoifikia katika mazungumzo baina ya vyama hivyo na Serikali kwa sasa, mikutano hiyo haitazuiliwa tena.
Hata hivyo hatua hii inakuja ukiwa umepita mwezi mmoja tangu Rais Samia akabidhiwa ripoti ya kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi.
Ambapo Mwenyekiti wa Kikosi Kazi hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema kuwa kilipendekeza mikutano ya hadhara iruhusiwe kufanyika kwa mujibu wa katiba na sheria.