Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Balozi Dkt. Stergomena Tax amesema Mipaka ya Tanzania iko katika hali ya usalama kwa kiasi kikubwa Pamoja na changamoto ndogo ambazo zinasikika katika baadhi ya maeneo.
Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Dar24 Media, Dkt. Stergomena amesema kwenye mipaka hapakosi matatizo madogo kwa kuwa tunatofautiana historia kwa kila nchi lakini kwa kutumia diplomasia ya ulinzi nchi inaweza kuzitatua changamoto hizo kwa njia ya mazungumzo bila kuathiri uhusiano na mataifa jirani.
Amewataka watanzania kuwa na amani kwa kuwa jeshi lipo imara na linaifanya kazi yake kwa wajibu na diplomasia ya ulinzi Pamoja na kushirikiana na nchi wanachama Jumuiya ya maendeleo ya Afrika na Serikali ya Tanzania inaendelea na mazungumzo na Malawi kuhusu tatizo la mpaka.
“Tuna changamoto ya mpaka wetu na Malawi lakini majadiliano yanaendelea na huwezi kuona matatizo yoyote kwasababu ya ukomavu wa diplomasia ya ulinzi tulionao,” amesema Dkt. Tax.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa, upande wa kusini mwa taifa katika mkoa wa Mtwara ambapo nchi inapakana na Msumbiji kumekuwa na changamoto ya ugaidi, kufuatia ripoti za matukio kadhaa yaliyohusishwa na vitendo vya kigaidi, lakini jeshi limeweza kudhibiti na kuimarisha ulinzi katika mpaka huo.
“Hali ya mipaka yetu ipo vizuri na salama hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi, Tanzania ni nchi mwanachama wa SADC hivyo changamoto zingine za kiusalama tunaunganisha nguvu na kushirikiana kuzitatua kijumuiya ila zile za ndani jeshi letu huwa inazimaliza,” ameongeza Dkt. Tax.
Mzozo wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi uliibuka mwaka 2011 baada ya Malawi kutoa leseni kwa kampuni ya British Surestream Petroleum Limited kuchimba mafuta na gesi katika ziwa Nyasa sehemu ya kilomita za mraba 20,000,, eneo ambalo Tanzania ilidai kuwa ni lake.
Mgogoro huo uliibua hofu mwaka 2012 baada ya Tanzania kusema kuwa ingelinda mipaka yake na kuzingatia sheria za kimataifa, na kuleta wasiwasi wa huenda taifa hilo likachukua hatua za kijeshi kulinda mpaka huo.
Tazama Mahojiano hayo kwa undani zaidi.