Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stergomena Tax amesema hafurahishwi na wanaohoji utendaji wa baadhi ya viongozi kwa kigezo cha jinsia.

Kiongozi huyo wa kwanza mwanamke katika Wizara hiyo nyeti, amesema mara zote amekuwa akiulizwa kuhusu changamoto za kuwa kuongoza maeneo nyeti kwakuwa yeye ni mwanamke, jambo ambalo anaona kuwa halipo sawa.

Ameyasema haya Katika Mahojiano maalum na Dar24 alipokua akizungumzia Uongozi wake na masuala na Ulinzi wa Nchi ya Tanzania na namna majeshi yanavyofanya kazi.

“Sijui kwanini wanawake huonekana tofauti, Sijawahi kusikia wa upande mwingine wakiulizwa wewe ni Waziri wa kwanza mwanaume unajisikiaje? Ifike wakati hili swali liachwe kuulizwa,” amesema Dkt. Tax wakati akihojiwa kwenye kipindi cha EXCLUSIVE cha Dar24 Media

“Kwenye jeshi hakuna mambo ya wewe ni mwanamke au wewe ni mwanaume, wote wanafanya kazi sawa na wote wanafanya vizuri kwenye majukumu yao, huwezi kuona tofauti kwenye kazi iliyofanywa na mwanamke au mwanaume,” aliongeza Dkt. Tax.

Hata hivyo kiongozi huyo amekiri kuwa mwanzoni alipata mshangao baada ya kupokea taarifa za kuteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi lakini baada ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alimtia moyo na ujasiri wa kuimudu nafasi hiyo na ameendelea kuchapa kazi.

“Nilipata kama woga kidogo na kujiuliza hivi ni mimi kweli nimeteuliwa kushika nafasi hii!, Ila nilijipa ujasiri na Mheshimiwa Rais alinipa moyo zaidi wakati ananiapisha aliposema anaamini ninaweza kazi na nikafanye kazi,”

Dkt. Stergomena Tax ni msomi aliyebobea kwenye masuala ya fedha na uchumi na amejijengea heshima kubwa kwenye uga wa kidiplomasia akiwahi kuhudumu katika wizara mbalimbali ikiwemo nafasi ya Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki na baadae Wizara ya fedha.

Kabla ya uteuzi wake wa nafasi ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Septemba 2021, Dkt Stergomena Tax alikuwa  Katibu Mtendaji Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), nafasi aliyohudumu kwa muda wa miaka nane.

Tuhuma za Ubadhirifu zamtoa kazini Mkurugenzi Masasi
TEITI yawapiga msasa viongozi kwenye uziduaji