Wawakilishi wa Kiungo kutoka nchini Uholanzi Donny van de Beek wamekuwa katika majadiliano na klabu kadhaa za Barani Ulaya kuhusu uwezekano wa Mchezaji huyo kuondoka Manchester United majira haya ya joto.
Van de Beek alijiunga na United Septemba 2020 akitokea Ajax Amsterdam, lakini hajawahi kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo chini ya makocha kadhaa.
Van de Beek amekuwa nyuma ya Bruno Fernandes katika safu ya kiungo na amekuwa akipambana na majeraha ya mara kwa mara ambayo yamedhoofisha kiwango chake nchini England.
Chini ya Erik ten Hag, kocha wa sasa wa United na kocha wa zamani wa Van de Beek kule Ajax, bado mambo hayajabadilika.
Van de Beek alipata jeraha Januari ambalo lilimweka nje kwa kipindi cha pili cha msimu uliopita na wakati amejiunga na mazoezi ya kujiandaa na msimu katika siku za hivi karibuni, United pia imemsajili Mason Mount kutoka Chelsea na hivyo, kupunguza uwezekano wa Van de Beek kupata nafasi msimu ujao.
Ingawa Ten Hag ana uhusiano mzuri na mchezaji huyo, lakini amewasha taa ya kijani kuondoka kwa Van de Beek kutoka katika klabu hiyo, na kambi ya mchezaji huyo inachunguza wapi atakwenda.
Van de Beek ana klabu kadhaa kutoka Serie A zinazowania huduma yake, huku Inter, Roma na Milan zikiwa tayari kutuma ofa, ingawa inafahamika kuwa yeye si chaguo la kwanza kwa timu yoyote kati ya hizi tatu.
Katika Ligi Kuu England, Wolves, Nottingham Forest na Crystal Palace zote zinafuatilia hali ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26.
Mabingwa wa Ligi ya Europa, Sevilla na Nice iliyonunuliwa na Sir Jim Ratcliffe, pia zinamwania, sawa na Celtic ya Brendan Rodgers.