Washtakiwa 14 waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka 41 yakiwemo ya kufanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu, kukwepa kodi na kuisababishia hasara ya Sh 31 Milioni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wamefutiwa kesi na kuwaachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa hao wameachiwa huru baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Silvester Mwakitalu kuwasilisha hati Mahakamani akieleza kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo.
Aidha uamuzi wa kuwafutia kesi na kuwaachia huru umetolewa leo Juni 22, 2021 na Hakimu Mkazi mwandamizi, Kassian Matembele wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo wakili amesema kuwa washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ( CPA) sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Baada ya upande wa mashtaka kueleza hayo, Hakimu alikubaliana na ombi hilo na kuwafutia mashtaka na kisha kuwaachia huru.
Waliofutiwa mashtaka katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 2/2021 ni Yusuph Mbuani, Joseph Magafu, Emmanuel Salu, Gogad Mayenga, Samson Akunahai, Husein John, Zacharias Paul, Dotto Shigula, Petro Simon, Emmanuel Sahani, Joseph Mathias, Massanja Paul, Aminiel Sangu na Emmanuel Lusinge.