Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika, limesema nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), imetangaza kumalizika kwa mlipuko mpya wa Ebola, baada ya hapo awali kuripotiwa kwa kesi moja, hatua ambayo inakuja wakati nchi jirani ya Uganda ikijaribu kudhibiti ugonjwa huo unaoendelea kuenea kwa kasi.
Nchini DRC, Virusi hivyo vilijitokeza tena wiki sita zilizopita katika jimbo la Kivu Kaskazini (mashariki mwa DRC), na inakuwa ni mara ya kwanza kudhibiti kwa haraka ugonjwa huo ambapo kwa nchi hiyo, imekumbwa na milipuko 15 ya Ebola tangu kugunduliwa kwake rasmi mwaka 1976.
WHO inasema, siku chache baada ya janga hilo kuthibitishwa mamlaka ya afya ilianza kampeni ya chanjo kulingana na mkakati wa ukanda na zaidi ya watu 500 walichanjwa, ikiwa ni pamoja na watu 350 wa mawasiliano na wafanyakazi wa mstari wa mbele ambao wanatajwa kushiriki utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa Ebola.
Mlipuko wa awali (mlipuko wa 14), uliosababisha vifo vya watu watano katika muda wa miezi mitatu magharibi mwa nchi hiyo, ulitangazwa kuwa umemalizika mapema Julai 4, 2022 tangazo linalokuja wakati Uganda, jirani wa DRC, “ikipambana kudhibiti mlipuko mwingine wa Ebola.
Kulingana na Wizara ya Afya ya Uganda, imesema kumekuwa na kesi 18 zilizothibitishwa tangu Jumatatu, Septemba 19, 2022 na kusababisha vifo 24, huku 18 vikitarajiwa kuweza kutokea kutokana na hali mbaya za wagonjwa waliolazwa, huku mgomo wa Madaktari wanaodai kukosa vifaa ukiongeza hatari zaidi.
Ofisi ya kanda ya WHO, inasema milipuko ya Ebola nchini DRC imesababishwa na ugonjwa wa Ebola “Zaire”, moja kati ya aina sita za jenasi ya Ebola na imefafanua kwamba Uganda inapambana na janga linaloendelea kwa kasi linalosababishwa na virusi vya Ebola vilivyotambuliwa kwa jina au aina ya Sudan.