Jiji la Dar es salaam, limetajwa kuwa na uhaba wa magari ya kusafirisha wagonjwa na wajawazito kutoka maeneo wanayoishi kufika hospitali, ikiwa ni pamoja na uhaba wa vitendea kazi na wahudumu wa afya.
Hayo yamesemwa na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa Rehema Madenge, wakati wa hafla ya kupokea magari 6 yaliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu duniani, UNFPA.
“Huwezi kuamini Dar es salaam inaangaliwa kama ina uwezo mkubwa lakini tunaathirika na idadi kubwa ya watu ambayo inatusababishia uhaba wa vitendea kazi mahospitalini. Sasa Mradi huu unakwenda kupunguza vifo vya wajawazito na Tunawashukuru UNFPA kwa kutufikiria hasa kwa wakati huu.” Amesema Madenge.
Ameongeza kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka kwa sababu wajawazito wengi wanapoteza uhai wakati wanaelekea kujifungua hivyo kikubwa ambacho serikali inafanya ni kuongeza usimamizi kuhakikisha huduma za mama na mtoto zinapatikana kwa uhakika.
“Tunapoteza wamama wengi wakati wanatoka maeneo wanayoishi kueleka hospitali, na tunasema kwamba Mjamzito hatakiwi kupoteza uhai wakati wa kujifungua.” Ameongeza Madenge.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA nchini Tanzania, Mark Schreiner, amesema shirika hilo linaenda sambamba na malengo ya serikali ya Tanzania ya kupunguza vifo vya wajawazito na kuhakikisha uzazi salama unawezekana kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha mahitaji muhimu yanapatikana katika kutoa huduma hizo.
“Tunaweka macho yetu mbele kuhakikisha malengo ya nchi yanafanikiwa kwa kushirikiana na nchi Zaidi ya 100 zinazoisaidia. Hivyo tunaishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendelea kukubali kuungana nasi kwa miaka 5 katika kupunguza changamoto za uzazi,” amesema Schreiner.
Naye Mganga mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Dkt Rashid Mfaume, amesema sababu ya kuchagua maeneo ya mijini ni kuwa idadi wa watu inaongezeka kutoka vijijini kwenda mijini na vituo vya huduma za afya haviongezeki.
“Tunaposema huduma za afya ya uzazi kwa wajawazito Watoto na vijana, kundi linaloathirika ni vijana kutokana na afya balehe hivyo magonjwa ya kuambukiza yanawasumbua. Magari haya yanaenda kuratibu afya ya uzazi kwa makundi yote tajwa.” Ameeleza Dkt Mfaume.
Felista Bwana ni Meneja wa miradi ya Afya ya uzazi, Mama, Watoto wachanga na vijana ambaye amesema UNFPA imeendelea kuwekeza katika eneo hilo ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na maboresho kwa makundi hayo na kuona kila mtu anapata haki ya msingi ya kuishi.
“Bado kuna ugumu wa uratibu wa shughuli hizi za afya ya uzazi na maeneo yanayojulikana kama mijini yana sehemu ambazo hazifikiki hivyo haya magari yanaenda kufanya kazi hiyo.” Amesema Bwana.
Magari hayo 6 yaliyogharimu milioni 570 kwa ajili ya usimamizi wa mradi wa miaka 5 wa kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na Watoto wachanga katika maeneo ya mjini yamekabidhiwa kwa mkoa wa Dar es salaam, Dodoma na wizara tatu ambazo ni Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu na TAMISEMI na taasisi ya TCCIH.