Mshambuliaji wa Azam FC Prince Dube, anatarajia kwenda Afrika kusini kwa matibabu, baada ya kupata majeraha ya mkono akiwa kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Young Africans, jana Jumatano (Novemba 25) Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Dube raia wa Zimbabwe, aliumia dakika ya 15 kwa kuvunjika mfupa wa mbele wa mkono wake wa kushoto unaoitwa Ulnar, hatua mabayo ilimlazimu kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Richard Djodi.
Ulnar ni mfupa unaoanzia kwenye kiwiko na kushuka hadi kwenye kidole cha mwisho.
Taarifa iliyotolewa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii ya Azam FC imeeleza kuwa, mshambliaji huyo ataondoka Dar es salaam Jumapili ya Novemba 29 kwa ndege ya Shirika la Kenya Airways (KQ).
“Atatibiwa kwenye Hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo Cape Town, chini ya daktari bingwa wa mifupa, Robert Nicolas.”
“Azam FC tumekuwa tukiitumia hospitali hii kutibia wachezaji wetu tangu mwaka 2011. Tunampa pole na kumtakia matibabu mema na kupona haraka, Prince Dube.” Imeeleza taarifa hiyo.