Klabu ya Mtibwa Sugar imekamilisha usajili wa Beki wa kulia David Kameta ‘Duchu’ kwa mkataba wa mwaka mmoja, ikiwa ni mpango kazi wa kukiboresha kikosi chao kwa msimu mpya wa 2022/23.
Mtibwa Sugar imedhamiria kuwa na kikosi imara msimu ujao, baada ya kunusurika kushuka Daraja kwa misimu miwili mfululizo, ikicheza michezo ya Mtoano ‘Play Off’.
Klabu hiyo ya Manungu-Turiani Morogoro, imemsajili Duchu, akitokea Geita Gold FC, ambayo aliitumikia kwa mkopo akitokea Simba SC msimu uliopita 2021/22.
Kuondoka kwa Beki huyo kunahusishwa na kusajiliwa kwa George Amani Wawa katika kikosi cha Geita Gold FC, na ilitarajiwa uwepo wake huenda ungeleta changamoto za ushindani wa nafasi ya beki wa kulia.
Awali Duchu alitajwa kuwa katika mazungumzo na viongozi wa Geita Gold FC, lakini siku moja baada ya kusajiliwa kwa Wawa, Mtibwa Sugar ikajitumbukiza katika mpango wa kumsajili na kufanikiwa.
Duchu aliwahi kucheza kwa mafanikio makubwa akiwa Lipuli FC ya Iringa ilipokua Ligi Kuu, hali ambayo ilimuwezesha kusajiliwa kwenye kikosi cha Simba SC.
Uwepo wa Shomari Kapombe, ulimkosesha nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha Simba SC, hatua ambayo ilipelekea kutolewa kwa mkopo Geita Gold FC.