Baada ya ukurasa wa pambano la ‘kibiashara’ la masumbwi kati ya Floyd Mayweather na Conor McGregor kufungwa, leo (usiku wa kuamkia kesho) dunia itashuhudia pambano linalotajwa kuwa la mwaka kati ya mabondia Canelo Alvarez (Mexico) na Gennady Golovkin aka Triple G (Kazakhstan).
Pambano hilo la ubingwa wa dunia wa uzito wa kati, litakalofanyika kwenye ukumbi wa T-Mobile Arena, Las Vegas nchini Marekani ni moja kati ya mapambano yaliyokuwa yakisubiriwa kwa hamu kwa miaka mingi kama ilivyokuwa kwa pambano kati ya Mayweather na Manny Pacquiao.
Tripple G, mbabe ambaye hajawahi kupoteza pambano kati ya mapigano 37 ameshinda mapambano 33 kwa kuwakata umeme wapinzani wake kabla ya raundi ya mwisho (knock outs). Nguvu na uzito wa ngumi yake ndio tishio kubwa kwa wapinzani wake.
Kwa upande wa Canelo, ni mbabe ambaye amewahi kupoteza pambano moja tu kati ya mapambano yake 51 na kupata sare ya pambano moja (49-1-1). Bondia huyo alipoteza pambano moja alipokutana na Mayweather katika uzito wa ‘Welterweight’.
Jana, mabondia hao walipima uzito huku kila mmoja akitamba kuweka historia kwa kushinda pambano hilo.
Wadau wamegawanyika katika mitazamo mbalimbali huku wengi wakimpa nafasi zaidi Canelo kutokana na kuwa na umri mdogo wa miaka 27 dhidi Tripple G mwenye umri wa miaka 35 pamoja na uharaka wake akiwa ulingoni.
Mayweather anaamini Canelo atamsimamisha Tripple G kabla ya raundi ya mwisho, lakini bondia Terence Crawford anampa nafasi zaidi Tripple G.