Kocha Mkuu wa Marumo Gallants Dylan Kerr amekiri wapinzani wake katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika Young Africans wana Mshambuliaji hatari Fiston Kalala Mayele, ambaye anaweza kuidhuru safu yoyote ya ulinzi ya timu anazokutana nazo.

Marumo Gallants tayari wameshawasili Dar es salaam-Tanzania kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Nusu Fainali utakaopigwa kesho Jumatano (Mei 10) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini humo, kuanzia saa kumi jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Kocha Dylan amesema: “Muda mwingine ni jambo zuri kujua mpinzani wako alivyo na ni Wachezaji gani hatari ili kuwa na namna bora ya kukabiliana nao”

“Mayele ni mchezaji tishio, sio tu kwetu hata kwa timu yoyote Afrika. Nitakuja kwa ajili ya Marumo na lengo letu ni kucheza fainali hivyo tutakuwa tayari kukabiliana na yoyote sio Mayele pekee yake bali timu nzima kwa ujumla ili tufanikishe mpango wetu”

“Ni miaka mingi kidogo tangu nifanye kazi Tanzania na Afrika mashariki lakini bado moyo wangu upo hapa, nimekuwa na marafiki ambao bado tunawasiliana”

“Tunajua tutakutana na mechi ngumu kwa sababu Uwanja ule (Kwa Mkapa) si sehemu nyepesi, Simba SC na Young Africans zinamashabiki wengi”

Marumo Gallants imefika hatua ya Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuitoa Pyramid ya Misri kwa ushindi wa jumla wa 2-1, huku Young Africans ikiiondoa Rivers United ya Nigeria kwa ushindi wa jumla wa 2-0.

Kocha Simba SC aomba radhi, kukutana na uongozi
Lisu afunguka uamuzi wa kulichukua gari Polisi