Uchunguzi umeanzishwa na Shirikisho la soka nchini Misri (EFA) baada ya kubaini kuwa vikombe kadhaa vimepotea kutoka makao makuu yake mjini Cairo, likiwemo kombe asili la Mataifa ya Afrika.
Misri ilipokea zawadi ya kombe hilo iposhinda michuano ya 2010, kwa kuwa ilikuwa imeshinda kombe la aina hiyo kwa mara ya tatu.
Kombe hilo ambalo mtindo wake ulitumiwa kwa mara ya kwanza mwaka 2002 baada ya Cameroon kupewa kombe la awali, kufuatia kushinda mara tatu shindano hilo, lilitolewa kwa EFA na shirikisho la soka la Afrika (CAF) baada ya kupata ushindi mara tatu mwaka 2006, 2008 na 2010.
Baada ya kushambuliwa kwa makao makuu ya EFA mwaka 2013, vikombe mbali mbali, likiwemo Kombe la Mataifa ya Afrika, vilihamishiwa kwenye chumba kingine maalum.
Hatahivyo, maafisa nchini humo walivitafuta vikombe hivyo hivi karibuni tu, baada ya uamuzi wa kukarabati lango la EFA ili vikombe vingi ambavyo Misri imevipata viwekwe eneo la kuingia kwa ajili ya maonyesho.
Uvamizi wa EFA na mashabiki wenye jazba miaka saba iliyopita wakati wa ghasia mjini Cairo kwa sasa ni suala linaoangaliwa huku maafisa wakijaribu kubaini ni lini na ni vipi vikombe hivyo vilichukulia.
” Kwa sasa EFA inachunguza ‘ kutoweka kwa vikombe ili kubaini kama vilikombe hivyo vya zamani vilichukuliwa wakati jengo lilipoungua…au kama vilipoteawakati jengo lilipovamiwa wakati wa tukio ,” – EFA.
Kulingana na sheria za CAF nchi ambayo timu yake inashinda kombe fulani la Mataifa ya Afrika mara tatu, timu hiyo inalimiliki moja kwa moja.
Kombe la sasa ambalo mtindo wake bado ni sawa na lile ambalo Misri ililitwaa, liko mikononi mwa Algeria, ambao walishinda taji la Kombe la Mataifa ya Afrika (mjini Cairo) mwaka jana.