Jumuiya ya Afrika Mashariki imeeleza kujivunia na miradi mikubwa na ya kimkakati inayotekelezwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba kukamilika kwake kutachochea ukuaji wa uchumi na biashara katika Jumuiya hiyo na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote akiwa na ujumbe wa Jumuiya hiyo walipotembelea mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere ambalo linatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2022.
Mhandisi Mlote ameeleza kuvutiwa na taarifa ya mradi huo kufadhiliwa na fedha za Watanzania na kumpongeza Rais Dkt Magufuli kwa maono hayo lakini pia kitendo cha kutoa zaidi ya ajira 5000 ambapo asilimia 90 ya waajiriwa ni Watanzania.
Awali ujumbe huo umetembelea mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa lengo la kijionea maendeleo ya ujenzi wa mradi huo na kueleza kufurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Tanzania.
Ujumbe huo umewasihi vijana wa Kitanzania waliopata fursa ya ujenzi wa reli kuendelea kujifunza kwa moyo na kwa kujituma, ili kupata maarifa na ujuzi wa kuendelea kutunza, kuendesha na kuendeleza mradi huo hata baada ya wataalamu kutoka kampuni inayohusika na ujenzi kuondoka nchi.
Mhandisi Mlote ametoa wito kwa Watanzania hasa ambao wanazunguka eneo la miradi hiyo kuitunza na kuilinda kwa kuwa manufaa yake ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa mazao shambani na bidhaa za viwandani, pamoja na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kati.