Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji Eden Hazard amepanga kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 32, huku ikidaiwa amegomea ofa kibao za kwenda kucheza soka nchini Saudi Arabia.
Mkali huyo aliyeitumikia timu ya taifa ya Ubelgiji mara 126 aliripotiwa pia kuzivutia timu za Vancouver Whitecaps, Nice, Marseille na timu yake ya zamani Lille, zote zikitajwa kuhitaji huduma yake akakipige kwenye vikosi vyao.
Taarifa zinaeleza kuwa Hazard amepanga kuachana ofa hizo na dhamira yake kuu ni kuachana kabisa na kucheza soka, huku jambo hilo likisubiri tu kutangazwa.
Hazard ameshindwa kucheza kwa ubora kama ule alionyesha alipokuwa akiitumikia Chelsea kwa miaka saba baada ya kujiunga na Real Madrid kwa ada ya Pauni 115 milioni mwaka 2019.
Ukiweka kando janga la majeruhi ambayo yamekuwa yakimwandama sana, kulikuwa na shida nyingine kwenye ufiti wa mchezaji huyo ikiwamo kuongezeka uzito.
Hazard alistaafu soka la kimataifa baada ya Ubelgiji kutolewa mapema kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizofanyika Qatar.
Akiwa hana timu yoyote tangu mkataba wake huko Real Madrid ulipofika ukomo Juni mwaka huu, imeelezwa mchezaji huyo anafikiria zaidi kustaafu kuliko kutafuta timu nyingine ya kwenda kuendeleza soka lake.