Meneja wa Mabingwa wa Soka Barani Ulaya Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema anatarajia kukabiliana na Manchester City iliyo tofauti sana kwenye hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Real Madrid iliibuka kidedea mbele ya Man City mwaka jana zilipokutana kwenye hatua kama hiyo na msimu huu miamba hiyo inakutana tena katika mechi ya kisasi.
Ancelotti alisema kuhusu Man City: “Wamebadilika kiasi, lakini bado wapo vizuri na wana nguvu ya mchezaji mmoja mmoja, wanaye straika Erling Haaland anayefunga sana mabao.
“Hawajabadilika staili yao ya uchezaji, wana Mshambuliaji mwenye nguvu, hivyo wamebadilika kiasi wanapokwenda kushambulia, lakini bado wanacheza soka la kumiliki mpira na kupandisha mpira mbele kwa mipango bila ya tatizo.”
“Yatupaswa kuwa bora zaidi yao. Tupo karibu kabisa na fainali na sifahamu kama wao wanapewa nafasi kubwa, hapa kila kitu kipo kwenye uzani sawa. Ngoja tuone.”