Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans umekamilisha usajili wa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Cameroon, Emmanuel Dikongue, kwa mkataba wa miaka miwili ili kuziba pengo la mshambuliaji anayeondoka Fiston Kalala Mayele.

Dikongue, mwenye umri wa miaka 28 anatarajia kutua nchini kesho Alhamis (Julai 27) akiwa anajiunga na Young Africans akitokea Klabu ya Canon Yaounde ya Cameroon, ambapo kabla ya hapo aliichezea Akonangui FC ya Equatorial Guinea.

Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa Dikongue anakwenda Young Africans kuziba pengo la Mayele ambaye muda wowote kibao cha kuagwa kitaonekana mitandaoni, akielekea kujiunga na Pyramids ya Misri.

“Ni kweli, uongozi umekamilisha usajili wa mshambuliaji kutoka Cameroon anayekuja kuchukua nafasi ya Mayele ambaye hakuwapo hata katika utambulisho wa juzi kwenye Tamasha la Kilele cha Siku ya Mwananchi.”

“Nadhani wakati wowote watamtangaza kwa sababu kila kitu kimeshakamilika juu yake hasa upande wa mkataba, kinachosubiriwa ni kuwasili kwake kwa ajili ya kumtangaza kabla ya kuanza kwa ligi na mechi za Ngao ya Jamii,” amesema mtoa taarifa hizi.

Akizungumza jijini Dar es salaam Afisa Habari wa klabu hiyo, Ally Kamwe, amesema mchakato wa usajili unaendelea baada ya Kocha Miguel Angel Gamond kuona wapi anatakiwa kuongeza nguvu baada ya mechi yao ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Amesema usajili unaendelea na bado kuna nafasi moja ya mchezaji wa kigeni ambapo mchakato huo unafanywa na Rais wao, Hersi Said, ili kuimarisha timu yao kuelekea msimu mpya.

“Tumeona wachezaji wapya tuliosajili na sasa bado nafasi moja ya mchezaji wa kigeni ambaye taratibu za usajili zinaendelea kukamilika kwa kushirikiana vizuri na Kocha Gamond (Miguel Angel),” amesema Kamwe.

Ruto, Odinga kuyajenga baada ya safari Tanzania
Pochettino aweka matumaini kwa Levi Colwill