Wachezaji wa kikosi cha England wenye asili ya bara la Afrika, usiku wa kuamkia leo walipata wakati mgumu wa kuvumilia changamoto za ubaguzi wa rangi, wakiwa katika jukumu la kupambana na Bulgaria katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Ulaya, mjini Sofia.
Mchezo huo uliomalizika kwa England kuchomoza na ushindi wa mabao sita kwa sifuri, ulilazimika kusimama mara mbili, kufuatia wachezaji wa The Three Lions kukerwa na matamshi ya mashabiki yaliyokua yakiwalenga wachezaji wenzao wenye asili ya bara la Afrika.
Mashabiki wa Bulgaria walisikika wakiigiza milio ya Gorila pindi wachezaji Raheem Sterling na Marcus Rashford walipomiliki mpira, jambo ambalo liliwakera wachezaji wote wa England.
Kocha wa England Gareth Southgate aliwatuliza wachezaji wake na mara kadhaa alikwenda kulalamika kwa mwamuzi kuhusu matukio hayo, ambayo kila kukicha yamekua yakipigwa vita michezoni.
Mchezo huo ulisimama dakika ya 43 baada ya Southgate kutoa malalamiko kwa mwamuzi kabla ya kuendelea. Awali ulisimama dakika ya 28.
Hata hivyo pamoja na kukutana na changamoto za kibaguzi, wachezaji wenye asili ya Afrika walifunga katika mchezo huo, Raheem Sterling (mabao mawili) na Marcus Rashford bao moja, huku mabao mengine yakipachikwa wavuni na Ross Barkley (mawili) na Harry Kane.
Wakati huo huo mwenyekiti wa chama cha soka nchini England (FA) Greg Clarke amethibitisha kuona tukio lingine ambalo halipewi nafasi katika michezo, kwa kusema mbali na ubaguzi wa rangi pia aliwashuhudia mashabiki wakionyesha ishara ya saluti yenye mlango wa kiasi.
“Niliona kundi la watu wapatao 50 wakiwa wamevaa mavazi ya rangi nyeusi wakitoa ishara mbaya ikiwemo saluti yenye mlengo na masuala ya kiasa,”alisema Mwenyekiti wa Chama cha Soka Greg Clarke.
Baadhi ya mashabiki wa Bulgaria wakionyesha saluti yenye mlengo na masuala ya kiasa
Matokeo ya michezo mingine ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Ulaya iliyochezwa usiku wa kuamkia leo:
Kundi A
Bulgaria 0 – 6 England
Kosovo 2 – 0 Montenegro
Kundi B
Lithuania 1 – 2 Serbia
Ukraine 2 – 1 Portugal
Kundi H
France 1 – 1 Turkey
Iceland 2 – 0 Andorra
Moldova 0 – 4 Albania