Mchezaji wa Simba SC Erasto Nyoni amethibitisha kuisaidia timu ya Majimaji FC ya Songea nauli ya kurejea nyumbani mkoani Ruvuma, baada ya kukwama kwa siku kadhaa jijini Dar es salaam.
Erasto ambaye ni Mwenyeji wa mji wa Songea mkoa wa Ruvuma, aliisaidia timu hiyo Jumapili (Februari 26), baada ya kurejea kutoka Uganda alikokuwa na kikosi cha timu yake, kwenye mchezo wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Vipers SC.
Mchezaji huyo mwenye sifa ya kucheza nafasi zaidi ya moja, amesema amewahi kupita hali kama hiyo, hivyo aliamua kuwapa msaada huo timu ya Majimaji ili kuwatia moyo, Wachezaji na viongozi.
“Sisi kama Kaka zao tunatakiwa tuwaoneshe na tuwape moyo ili waweze kupambana maana kazi yetu ya mpira ni kazi ngumu sana unatakiwa usikate tamaa uwe Mvumilivu sasa uvumili hauji tu hivihivi lazima kuna Watu wawe wanakupa hiyo nguvu”
“Nimeshawahi kupitia hii hali ndio maana ilipotokea ikanisukuma ikanisukuma kufanya hivi kwasababu imeshwhi kunitokea” amesema Erasto
Majimaji FC ilikwama jijini Dar es salaam baada ya kumaliza mchezo wake wa Ligi Daraja la Pili dhidi ya African Lyon na Dar City FC, kutokana na kukosa pesa za nauli ya kurudi Songea-Ruvuma.