Meneja wa Manchester United Erik ten Hag ametoa angalizo kwa Uongozi wa Klabu hiyo kwa kuwaambia wanahitaji kufanya uwekezaji mkubwa kipindi cha usajili wa majira ya joto, tofauti na hapo mambo yatakuwa magumu.
Manchester United imemaliza msimu huu ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Premier, huku mchezo wa mwisho juzi Jumapili (Mei 28) ikiifunga Fulham mabao 2-1.
United wamehitishima msimu huu wakiwa na Ten Hag, wakimaliza ndani ya Top Four, huku timu hiyo ikitwaa Carabao Cup, wikiendi inatarajiwa kucheza Fainali ya Kombe la FA.
Wakati wakielekea majira ya joto, Manchester United, tayari imemtaja Harry Kane kama namba moja kati ya wachezaji ambao wanataka kuwasajili.
Kocha huyo amesema: “Klabu inafahamu kuwa kama unataka kucheza ndani ya nne bora katika ligi hii lazima uwekezaji uwe wa maana, tofauti na hapo inakuwa ngumu kupata nafasi kwa sababu klabu nyingine zitapambana.
“Hali hiyo tuliiona majira ya baridi (Januari mwaka huu) klabu zote zilifanya uwekezaji, ila sisi hatukufanya na tukapambana kufika hapa.
Tupo sehemu nzuri, lakini hatupo pale ambapo tunapahitaji, kuna nafasi ya kufanya vizuri kama timu na mchezaji mmojammoja, hilo tumeweza kulionesha msimu huu, lakini wakati ujao uwekezaji unahitajika.”
Kocha huyo amesisitiza kuwa, Man United mpango wake ni kuzima ndoto za Man City kuelekea fainali ya FA.
“Nafikiri kuwa siku zote kuna nafasi katika soka. Historia inaonesha kuwa Januari tuliwafunga na huko nyuma tumewafunga sana.
Hawa wachezaji wangu wanacheza katika kiwango cha juu kwa sababu wanajua nini wanahitaji, japo tunajua tunaenda kucheza na timu bora, hatuhitaji visingizio,” amesema