Mshambualiji wa Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City Erling Haaland amesaini dili kabambe lenye thamani ya Pauni Milioni 20, likihusisha viatu vyake vya kuchezea vilivyotengenezwa na Kampuni ya Nike.

Mkataba huo utazidi miaka 10 na Haaland atapata fursa ya kupita kwenye nyayo za shujaa wake, Ronaldo kama sura kwenye Namba 9.

Mshambuliaji huyo Raia wa Norway mwenye umri wa miaka 22, mara ya kwanza alijiunga na Kampuni ya Nike akiwa na umri wa miaka 14, lakini mkataba wake huo wa awali ulifika kikomo Januari 2022.

Jambo hilo lilimfanya avae viatu vya aina tofauti, ikiwamo Puma Ultras wakati alipotambulishwa Man City na kisha alivaa adidas X Speedportals mechi ya Ngao ya Jamii.

Lakini, amerudi kwenye viatu vya Nike Mercurial Vapors katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu England na kuziingiza kwenye vita kali kampuni tatu za viatu kumfukuzia.

Sasa, vita hiyo imefika ukomo baada ya Haaland kunaswa na kampuni hiyo ya nchini Marekani.

Kampuni ya Nike inamiliki mastaa kibao wa maana ikiwamo Kylian Mbappe, Marcus Rashford, Harry Kane, Kevin De Bruyne na Cristiano Ronaldo kwa kuwataja kwa uchache.

Haaland ameendelea kutamba kwa kutikisa nyavu na hadi sasa amefunga mabao 42 katika michezo 37 aliyocheza chini ya Pep Guardiola na haonekani kupoa kwenye kutikisa nyavu.

TARI – Dakawa yapatiwa Milioni 30 kusafisha Mbegu za asili za Mpunga
Pascal Wawa amwagia sifa Fiston Mayele